Matumizi makubwa katika kipindi cha sikukuu
2024-03-18 07:57:44| CRI

Mwezi wa Ramadhani umeingia na kwa sasa tunaamini kwamba waumini wengi wa dini ya kiislamu mbali na kutekeleza nguzo hii muhimu sana pia watakuwa kwenye pirikapirika za kuandaa futari pamoja na maandalizi ya sikukuu ya Eid. Maandalizi haya kama tunavyofahamu kwamba yanahitaji pesa. Katika kipindi hiki gharama za matumizi kwenye familia za waislamu huwa zinapanda maradufu ama zaidi. Lakini je umewahi kujiuliza utakabiliana vipi na gharama hizi bila kujikuta upo kwenye mzigo mkubwa wa madeni?

Kwa kawaida katika mwezi wa Ramadhani na sikukuu yake ni wakati wa roho kutamani, hivyo utakuta kwenye nyumba za waislamu wanapika vyakula vya aina mbalimbali kwaajili ya futari na daku. Hivyo baba au mama katika kipindi huwa wanakuna vichwa sana ili kuhakikisha mlo maridadi kabisa unakuwepo mezani katika mwezi mzima, na kama haitoshi kuhakikisha nyumba inabadilika kabisa kwa mapambano, n ahata kuwatafutia watoto nguo mpya za sikukuu. Lakini usipokuwa na mpango unaofaa katika kipindi hiki huenda ukajikuta unatumia pesa nyingi bila kujijua. Hii ina maana kwamba hadi unamaliza ramdhani na sikukuu yake unaweza kujikuta kwamba umejaa madeni. Hivyo leo katika kipindi cha ukumbi wa wanawake tutaangalia gharama kubwa za matumizi zinazozikabili familia katika kipindi cha Ramadhani na sikukuu.