Viongozi wa nchi za Afrika ya Kati wamekutana jumamosi iliyopita mjini Bangui, mji mkuu wa Jamhuri ya Afrika ya Kati, kusherehekea kumbukumbu ya miaka 30 tangu kuanzishwa kwa Jumuiya ya Kiuchumi na Kifedha ya Nchi za Afrika ya Kati (CEMAC).
Mkutano huo umelenga kutathmini mafanikio yaliyopatikana na kupanga mikakati ya kuboresha maingiliano ya kikanda, huku msisitizo ukiwa katika kukabiliana na changamoto za kiuchumi na fursa za ukuaji.
Kutokana na uwekezaji mkubwa na utaalamu kutoka China, nchi wanachama wa Jumuiya hiyo wameshuhudia ujenzi wa miradi mikubwa ya miundombinu katika sekta ya uchukuzi, ikiwemo ujenzi wa Bandari ya Kina Kirefu ya Kribi katika mji wa Kribi, kusini mwa Cameroon, ambayo imejengwa na kampuni ya Uhandisi wa Bandari ya China (CHEC).
Meneja mkuu wa kampuni ya CHEC kanda ya Afrika ya Kati, Xu Huajiang amesema, utandawazi na maingiliano ya kikanda vimekuwa ni mwelekeo wa kawaida wa maendeleo, na vinapaswa kukumbatiwa na nchi za Afrika.