Niger yafuta makubaliano ya kijeshi kati yake na Marekani
2024-03-18 14:10:24| cri

Niger imesitisha makubaliano ya kijeshi yaliyoruhusu wanajeshi wa Marekani kutumwa nchini humo. Hatua hiyo imefikiwa katika wiki ambayo wajumbe kutoka Marekani walikuwa mjini Niamey kwa mazungumzo na uongozi wa kijeshi wa nchi hiyo. Marekani ilitumia kituo chake cha kijeshi nchini Niger kufuatilia shughuli za kikanda za vikundi cha jihad.

Hatua hiyo ya serikali ya Niger iliyo madarakani tangu Julai mwaka jana, inakuja wakati nchi hiyo inaimarisha uhusiano na Russia na baada ya wanajeshi wa Ufaransa kutimuliwa mwezi Desemba.

Msemaji wa jeshi la Niger Col. Amadou Abdramane amesema uwepo wa Marekani katika eneo la Jamhuri ya Niger ni kinyume cha sheria na unakiuka sheria zote za kikatiba na kidemokrasia ambazo zingehitaji watu wenye mamlaka kuulizwa kuhusu kuwekwa kwa jeshi la kigeni katika eneo lake.

Pia amedai ujumbe wa Marekani uliishutumu Niger kwa kufanya makubaliano ya siri ya kutoa uranium kwa Iran. Kanali Abdramane ameeleza kuwa shutuma hizo ni za "kijinga" na "zinakumbusha vita ya pili ya Iraqi". Pia amesema Marekani imetoa pingamizi kuhusu washirika ambao Niger imewachagua.