Afya na wanawake na watoto
2024-04-04 08:11:20| CRI

Hivi sasa katika dunia nzima, haki ya afya ya mamilioni ya watu inazidi kuwa hatarini. Magonjwa na majanga yanaonekana kuwa sababu za vifo na ulemavu. Migogoro nayo pia inaharibu maisha ya watu, inasababisha vifo, maumivu, njaa na matatizo ya kisaikolojia. Matumizi makubwa ya mafuta ya magari yanayosababisha hewa ya ukaa na kupelekea msukosuko wa hali ya hewa, pia yanaondoa haki yetu ya kupumua hewa safi, huku uchafuzi wa hewa wa ndani na nje ukigharimu maisha kila baada ya sekunde 5.

Hivyo Baraza la WHO linalojishughulisha na Uchumi wa Afya kwa wote limegundua kuwa takriban nchi 140 zinatambua afya kama haki ya binadamu katika katiba yao. Hata hivyo nchi hizi hazipitishi wala kutekeleza sheria za kuhakikisha kuwa watu wao wana haki ya kupata huduma za afya. Hii inaonesha ukweli kwamba takriban watu bilioni 4.5, ambao ni zaidi ya nusu ya idadi ya watu duniani hawapati huduma muhimu zilizo kikamili. Ili kukabiliana na changamoto za aina hii, kaulimbiu ya Siku ya Afya Duniani mwaka 2024 ni 'Afya yangu, haki yangu'.

Kaulimbiu ya mwaka huu imechaguliwa ili kutetea haki ya kila mtu na kila mahali kupata huduma bora za afya, elimu, na taarifa, pamoja na maji safi ya kunywa, hewa safi, lishe bora, makazi bora, mazingira bora ya kazi na kuwa uhuru dhidi ya ubaguzi. Kwa kuonelea hilo, katika kipindi cha Ukumbi wa wanawake leo tutajadili afya na wanawake na watoto.