Kenya yazindua mpango wa kimkakati kukuza matumizi ya nishati ya nyuklia
2024-03-19 08:32:33| CRI

Kenya imezindua mpango wake wa kimkakati jumatatu ili kukuza matumizi ya amani ya teknolojia ya nyuklia katika uzalishaji wa umeme.

Katibu mkuu wa Wizara ya Nishati na Mafuta, Alex Wachira amesema mpango huo unatoa mwongozo wa kuendeleza miundo mbinu ya kujenga, kuendesha, kulinda na kusimamisha vituo vya nyuklia kwa usalama. Amesema mpango huo umeweka hatua za kiutendaji kuhakikisha Kenya inaanza ujenzi wa kituo chake cha kwanza ifikapo mwaka 2027, ambacho kitaanza kufanya kazi ifikapo mwaka 2034.

Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Nyuklia na Nishati nchini humo Justus Wabuyabo amesema, mkakati huo utahakikisha Kenya inafuata mikataba na majukumu ya kimataifa kusimamia matumizi ya nyuklia, ulinzi wa mionzi, usafirishaji wa vifaa vya mionzi na takataka za nyuklia.