Mashirika ya Umoja wa Mataifa yatoa huduma za afya kwa zaidi ya Wasomali milioni 5
2024-03-19 08:34:20| CRI

Shirika la Idadi ya Watu la Umoja wa Mataifa (UNFPA) na Shirika la Afya Duniani (WHO) yamesema, yametoa vifaa na huduma ya afya kwa zaidi ya watu milioni 5 katika maeneo yaliyoathiriwa na ukame nchini Somalia.

Mashirika hayo yamesema fedha zilizotolewa na Kituo cha Misaada ya Kibinadamu na Ulinzi wa Raia cha Umoja wa Ulaya pia zimeisaidia Somalia na mikoa mingine minne kutoa huduma za afya na lishe kwa watu waliokimbia makazi yao.

Katika taarifa yao ya pamoja iliyotolewa jana mjini Mogadishu, mji mkuu wa Somalia, Mashirika hayo yamesema, mradi huo wa ufadhili wa miaka miwili wa Umoja wa Ulaya unalenga kuongeza huduma za afya na lishe katika kambi za wakimbizi wa ndani na jamii zinazowahudumia, na kukabiliana na mahitaji ya wanawake wajawazito na wanaonyonyesha, wazee, na watoto walio na umri wa chini ya miaka mitano katika maeneo yaliyoathiriwa na ukame.