Biashara kati ya Rwanda na Zimbabwe yaongezeka kwa asilimia 50
2024-03-19 10:29:41| cri

Jumuiya za wafanyabiashara wa Rwanda na Zimbabwe zimejitolea kuendelea kuimarisha uhusiano wa kibiashara, kufuatia ongezeko la asilimia 50 la biashara lililosajiliwa tangu juhudi za kwanza za ushirikishwaji wa biashara kati ya pande mbili.

Hili limebainishwa kwenye kongamano la tatu la Biashara la Rwanda na Zimbabwe lililoanza jana mjini Kigali, likiwaleta pamoja viongozi wa wafanyabiashara, wawekezaji, wakuu wa sekta hiyo, na maofisa wa serikali ili kuangalia maeneo zaidi ya ushirikiano wa kibiashara na uwekezaji.

Kongamano hilo la siku mbili ni jukwaa la mabadilishano na mitandao kati ya jumuiya za wafanyabiashara wa nchi hizo mbili, lenye lengo la kuimarisha makubaliano yaliyopo baina ya nchi hizo mbili, na kuandaa njia mpya za uwekezaji na kuweka mifumo wezeshi.