Umoja wa Mataifa waripoti kuongezeka kwa vurugu nchini Sudan Kusini
2024-03-19 08:35:11| CRI

Tume ya Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini (UNMISS) imesema, watu 862 wameuawa, kujeruhiwa, kutekwa nyara ama kuhusishwa na uhalifu wa kijinsia unaohusiana na mapigano katika robo ya pili ya mwaka jana nchini Sudan Kusini.

Ripoti ya Tume hiyo inayojumuisha miezi ya Oktoba mpaka Desemba mwaka jana, imeorodhesha matukio 233 ya mapigano nchini Sudan Kusini, huku watu 862 wakiathiriwa, ambako watu 406 wameuawa, 293 kujeruhiwa, 100 kutekwa nyara, na 63 kufanyiwa uhalifu wa kijinsia unaohusiana na mapigano.

Mjumbe maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa na kiongozi wa UNMISS, Nicholas Haysom amesema, mapigano ya kikabila yameendelea kusababisha madhara makubwa kwa jamii za nchini humo. Ameongeza kuwa, Tume hiyo inafanya kila linalowezekana kuzuia mapigano na kujenga amani katika maeneo yaliyoathiriwa, lakini juhudi zaidi zinapaswa kufanywa na mamlaka katika ngazi za kitaifa, mikoa na wilaya ili kusuluhisha migogoro iliyopo.