WHO yahimiza uwekezaji wa kifanisi ili kukabiliana na magonjwa ya kinywa barani Afrika
2024-03-20 08:33:05| cri

Mkurugenzi wa Shirika la Afya Duniani (WHO) kanda ya Afrika Bibi Matshidiso Moeti amesema, mzigo unaoongezeka wa magonjwa ya kinywa barani Afrika unaweza kupunguzwa kwa kuwekeza katika elimu ya usafi, rasilimali watu na hatua madhubuti za kliniki.

Bibi Moeti amesema, bara la Afrika ni kitovu cha magonjwa ya kinywa kama vile kuungua kwa meno, ugonjwa wa fizi na upotevu wa meno, ambayo huathiri asilimia 44 ya watu barani humo. Amelaani uwekezaji mdogo katika afya ya kinywa kote Afrika, ambapo asilimia 70 ya nchi za Afrika zilitumia chini ya dola moja ya Marekani kwa kila mtu kwa gharama za matibabu mwaka 2019.

Bibi Moeti pia amesema, magonjwa mengi ya kinywa yanaweza kuzuiwa kwa kuepuka mambo ya hatari kama vile matumizi ya tumbaku na pombe, kutumia vyakula visivyo na sukari, na kusafisha meno kwa dawa ya meno yenye floridi mara mbili kwa siku.