Umoja wa Afrika wajadili kuunda tume ya ufuatiliaji baada ya kuondoa kikosi chake nchini Somalia mwaka 2025
2024-03-20 08:34:31| CRI

Umoja wa Afrika unajadili kuunda tume ya ufuatiliaji baada ya kuondoa rasmi kikosi chake nchini Somalia itakapofika mwezi Desemba mwaka huu.

Mwakilishi maalum wa Umoja huo nchini Somalia, El-Amine Souef amethibitisha katika taarifa iliyotolewa jana jumanne mjini Mogadishu, mji mkuu wa Somalia, kwamba Tume ya Mpito ya Umoja wa Afrika nchini Somalia (ATMIS) itaondoka nchini humo mwezi Desemba, lakini kutokana na ombi rasmi lililotolewa na Somalia, tume ndogo ya ufuatiliaji inaandaliwa.

Kauli ya mwakilishi huyo inakuja baada ya kutembelea Dhobley, mkoani Jubaland, kwa lengo la kuunga mkono operesheni za ulinzi wa amani na kuwapa moyo askari wa kulinda amani wa Umoja wa Afrika walioko kusini mwa Somalia.

Umoja wa Afrika utaondoa askari 5,000 kutoka Somalia na kukabidhi zaidi ya kambi 13 za jeshi kwa Vikosi vya Usalama vya Somalia wakati wa awamu ya kwanza na ya pili ya kuondoka nchini humo kama ilivyoahidiwa mwaka jana.