China yatoa wito kwa pande zote mbili kwenye mzozo nchini Sudan kusitisha vita wakati wa mwezi mtukufu wa Ramadhani
2024-03-21 08:36:51| cri

Naibu mwakilishi wa kudumu wa China katika Umoja wa Mataifa, Balozi Dai Bing amezitaka pande zote mbili kwenye mzozo wa Sudan kutekeleza matakwa ya azimio namba 2724 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, kufikia makubaliano ya kusitisha vita wakati wa mwezi mtukufu wa Ramadhani haraka iwezekanavyo, kuepusha vifo vya raia, na kuzuia kuenea zaidi kwa mzozo huo kwa nchi jirani.

Akizungumza jana katika kikao cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu suala la chakula nchini Sudan, Balozi Dai amesema mzozo nchini Sudan unaendelea kuongezeka huku hali ya kibinadamu ikiendelea kuzorota, ambapo watu milioni 18 wanakabiliwa na njaa, na matatizo ya usalama wa chakula ni makubwa katika maeneo mengi. Amesema China inathamini kazi ya mashirika ya kibinadamu ya Umoja wa Mataifa, inakaribisha mamlaka ya Sudan kufungua vituo vingi vya kibinadamu na kushirikiana kikamilifu kutoa misaada ya kibinadamu, na kutoa wito kwa pande zote nchini Sudan kuendelea kuhakikisha ufikiaji wa haraka, salama na usio na vikwazo vya kibinadamu.

Bw. Dai pia alisema, jamii ya kimataifa, hasa wafadhili wa jadi, wanapaswa kuwajibika, kuongeza msaada wa kifedha na chakula, kujaribu kupunguza athari za migogoro katika maisha ya watu, na kuepuka maafa makubwa zaidi ya kibinadamu.