Kampuni zaidi za China zatafuta fursa za uwekezaji nchini Tanzania
2024-03-21 08:37:42| CRI

Kampuni 60 za uwekezaji kutoka China zitashiriki katika mkutano wa uwekezaji kati ya China na Tanzania utakaofanyika jijini Dar es Salaam tarehe 27 mwezi huu.

Ofisa katika Kituo cha Uwekezaji Tanzania, Diana Mwamanga amesema, mkutano huo unalenga kutangaza fursa za uwekezaji nchini Tanzania kwa wawekezaji kutoka China. Amesema wajasiriamali 60 kutoka mji wa Jinhua, mkoa wa Zhejiang nchini China, watatembelea Tanzania kuanzia tarehe 24 hadi 29 mwezi huu, kwa lengo la kuimarisha mawasiliano na mabadilishano kati ya pande hizo mbili na kutafuta fursa za uwekezaji kwa ajili ya ushirikiano.

Mwenyekiti wa Bustani ya Viwanda ya China na Tanzania jijini Dar es Salaam, Janson Huang amesema, fursa kubwa za uwekezaji zitajumuisha viwanda katika madawa, vitambaa na nguo, mashine za kilimo, vifaa vya ujenzi pamoja na uchimbaji madini na vifaa vya ulinzi wa mazingira.

Amesema katika mkutano huo, zaidi ya kampuni 120 za Tanzania zitapata fursa ya kufanya mikutano ya kibiashara na wenzao wa China.