Vyama vya siasa katika serikali ya mpito ya umoja ya nchini Sudan Kusini vinapaswa kufanya majadiliano ya kiujenzi ili kukubaliana katika utekelezaji wa majukumu muhimu ambayo hayajashughulikiwa ndani ya miezi minane iliyobaki kabla ya kufanyika kwa uchaguzi mkuu.
Hayo yamesemwa na Tume ya Pamoja ya Usimamizi na Tathmini (RJMEC) nchini Sudan Kusini, inayosimamia makubaliano mapya ya amani ya mwaka 2018. Tume hiyo imesema kuna haja ya mwongozo wa wazi na wa kivitendo wa kisiasa kutoka kwa wakuu wa Serikali ya Mpito ya Umoja wa Kitaifa (RTGoNU) na pande husika katika makubaliano hayo kuhusu njia za kutekeleza na kukamilisha majukumu yaliyosalia kabla ya uchaguzi.
Sudan Kusini inatarajiwa kufanya uchaguzi mkuu mwezi Desemba, kabla ya kumalizika kwa kipindi cha mpito mwezi Februari, mwaka ujao.