Ethiopia yatoa wito wa ushirikiano imara zaidi na China
2024-03-22 08:37:43| CRI

Mkurugenzi mtendaji wa Idara ya Mashariki ya Kati, Asia na Pasific katika Wizara ya Mambo ya Nje ya Ethiopia, Gebeyehu Ganga ametoa wito wa kutekeleza zaidi ushirikiano kati ya China na Ethiopia kupitia majukwaa na mapendekezo ya pamoja.

Akizungumza katika warsha ya Pendekezo la Ukanda Mmoja, Njia Moja (BRI) iliyofanyika mjini Addis Ababa, mji mkuu wa Ethiopia jumatano wiki hii, Ganga amesema uhusiano wa nchi hizo mbili umedumu kwa miongo mitano, na kuna haja ya kuimarisha ushirikiano na kudumisha urafiki kati ya nchi hizo.

Amesema Ethiopia inaahidi kuendeleza zaidi ushirikiano na China kwa kuboresha fursa zinazotokana na Pendekezo la Ukanda Mmoja, Njia Moja na mapendekezo mengine yanayotolewa na China.

Amesema kama kielelezo cha wazi cha uhusiano unaoendelea kupanuka kati ya China na Ethiopia, nchi hizo mbili zimeinua uhusiano wao na kuwa uhusiano wa kimkakati wa pande zote mwezi Oktoba mwaka jana, hatua inayoashiria kufungua ukurasa mpya katika uhusiano wa pande mbili hizo.