Waziri wa Jamhuri ya Afrika ya Kati asema miradi ndani ya mfumo wa ushirikiano kati ya China na Afrika ni ya kivitendo
2024-03-22 08:50:03| cri

Waziri wa Vifaa na Ujenzi wa Umma wa Jamhuri ya Afrika ya Kati, Bw. Eric Rekos-Kamo, na Waziri wa Kilimo na Maendeleo ya Vijijini wa nchini humo Bw. Gusimara Amza, wamesema kwa kauli moja mjini Bangui kwamba, miradi ndani ya mfumo wa ushirikiano kati ya China na Afrika imeisaidia Afrika kujikwamua katika umaskini.

Mawaziri hao wamesema wanatumaini kuwa ushirikiano kati ya Jamhuri ya Afrika ya Kati na China utaendelezwa zaidi katika sekta mbalimbali zikiwemo kilimo, miundombinu, matibabu na afya.

Bw. Amza amesema, miradi mikubwa ya kilimo inayotekelezwa na China nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati sio tu inakidhi mahitaji ya kimsingi ya watu wa Jamhuri ya Afrika ya Kati, bali pia inatoa fursa za ajira kwa watu wa eneo hilo na imekuwa na manufaa kwa nchi hiyo.

Naye Waziri Rekos-Kamo anakanusha madai kutoka kwa baadhi ya nchi za Magharibi kuwa China inafuata "diplomasia ya mtego wa madeni" barani Afrika. Amesema tofauti na baadhi ya nchi za Magharibi, ushirikiano wa China na Afrika hauna masharti yoyote, na matokeo halisi yanaonekana.