Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa limepiga kura kupitisha mswada wa azimio la kwanza kuhusu akili bandia (AI) ili kuhakikisha teknolojia hii mpya inaweza kunufaisha nchi zote, kuheshimu haki za binadamu na kuwa salama, ya kutegemeka na ya kuaminika.
Habari zinasema mswada wa azimio hili unalenga kuondoa tofauti ya kidijitali kati ya nchi zilizoendelea na zinazoendelea, na kuhakikisha kuwa pande hizo mbili ziko katika usawa wakati wa kujadili masuala ya AI. Pia inalenga kuhakikisha kuwa nchi zinazoendelea zina teknolojia na uwezo wa kutumia AI.
Mswada wa azimio hilo unakubali kuharakishwa kwa maendeleo na matumizi ya AI na inasisitiza hitaji la dharura la kufikia makubaliano ya kimataifa kuhusu mifumo ya AI iliyo salama, ya kutegemeka na kuaminika. Azimio hilo pia linakubali kwamba usimamizi wa mifumo ya AI ni endelevu, na inahitaji mjadala zaidi kuhusu njia zinazowezekana za usimamizi.
Habari zinasema China ilishiriki kwenye maandalizi ya mswada huo uliopendekezwa na Marekani.