Nchi za Afrika zalaani shambulizi la kigaidi katika jumba la muziki mjini Moscow
2024-03-25 08:47:23| CRI

Nchi mbalimbali za Afrika zimelaani shambulizi la kigaidi lililotokea ijumaa kwenye jumba la muziki la Crocus kaskazini-magharibi mwa mji wa Moscow, na kutoa salamu za rambirambi na mshikamano wao na Russia.

Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika (AU) Bw. Moussa Faki Mahamat amesema ameshtushwa shambulizi hilo na kulilaani vikali. Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ya Tanzania imetoa taarifa ikitoa salamu za rambirambi kwa serikali na watu wa Russia, na kulaani vikali kitendo hicho cha kinyama.

Taarifa ya wizara ya Mambo ya Nje na Masuala ya Diaspora ya Kenya, imelitaja shambulio hilo la kigaidi kuwa la kinyama, lisilo na maana na linalopingana na kanuni zote za kimsingi za ubinadamu.

Namibia, Ethiopia, Afrika Kusini na Somalia pia kwa nyakati tofauti zimetoa taarifa zikilaani vikali shambulizi hilo.