Somalia yashuhudia maendeleo makubwa katika kutokomeza ugonjwa wa kifua kikuu
2024-03-25 08:57:01| CRI

Somalia imesema inapiga hatua kubwa kuelekea lengo la kimataifa la kutokomeza ugonjwa wa kifua kikuu (TB) hadi kufikia mwaka 2030, huku ikitaka uwekezaji zaidi kusaidia kudumisha mafanikio yaliyopatikana.

Meneja wa mpango wa kupambana na kifua kikuu katika wizara ya huduma za afya na binadamu ya Somalia Bw. Mohamed Jafar, amesema mpango wa kupambana na TB wa Somalia umestahimili majanga ya tabianchi, kukosekana kwa usalama na janga la COVID-19, na kushuhudia kiwango cha mafanikio ya tiba kikifikia asilimia 87. Bw. Jafar pia amesema, katika miongo miwili iliyopita, kumekuwa na kiwango cha kupungua kwa wagonjwa wa TB cha asilimia 14, na ongezeko katika idadi ya vituo vya tiba ya TB kutoka 7 hadi 109.

Bw. Jafar amesema hayo mjini Mogadishu wakati wa maadhimisho ya siku ya kimataifa ya kifua kikuu inayoadhimishwa Machi 24 kila mwaka.