Watu wanne wafariki Nairobi kufuatia mvua kubwa
2024-03-26 09:26:31| CRI

Polisi wa Kenya wamethibitisha kuwa watu wasiopungua wanne wamefariki ndani ya saa 24 baada ya mvua kubwa kuikumba Nairobi.

Kamanda wa Polisi kaunti ya Nairobi Adamson Bungei amesema wahanga hao ni pamoja na askari polisi mmoja aliyekuwa akijaribu kuwaokoa wakazi waliokwama huko Kamukunji na mwili wake bado haujapatikana. Kwa mujibu wa kamanda huyu, nyumba zilizoko karibu na mito na mifereji katika mji huo pia zimesombwa na maji na watoa huduma za dharura wamepelekwa katika maeneo mbalimbali yaliyoathirika ili kuangalia hali ya wakazi wa maeneo hayo.

Serikali ya kaunti ya Nairobi imesema inashughulikia mambo husika ikishirikiana na serikali kuu, polisi na Chama cha Msalaba Mwekundu, na imeanzisha mpango wa dharura kukabiliana na maafa hayo.