Mkutano wa masoko ya kaboni 2024 wafanyika Nairobi
2024-03-27 09:12:04| CRI

Mkutano wa masoko ya kaboni 2024 umefanyika mjini Nairobi, ukiwa na lengo la kuhimiza biashara ya kaboni barani Afrika.

Mkutano huo wa siku mbili umewaleta pamoja washiriki zaidi 200 wakiwemo maofisa wa serikali, wafadhili na waendelezaji miradi kutoka sehemu mbalimbali duniani, ambao watabadilishana ujuzi kuhusu kuhimiza fursa za masoko hayo barani Afrika.

Akifungua mkutano huo, Waziri Mkuu wa Kenya Musalia Mudavadi amesema, Kenya inaweza kupunguza na kuepuka uzalishaji wa tani milioni 30 za kaboni kila mwaka, na inatarajia kupata dola za kimarekani milioni 600 kupitia biashara ya kaboni ifikapo mwaka 2030.

Ameongeza kuwa japo uzalishaji wa kaboni barani Afrika ni mdogo, bara hilo linaathiriwa vibaya na mabadiliko ya tabia nchi, lakini bado kuna fursa ambapo Afrika sasa inakumbatia fursa ya ukuaji endelevu wa uchumi na viwanda vya kijani ikiwa na maliasili nyingi za nishati, ardhi kubwa ya kilimo na mifumo anuwai ya ikolojia ya ardhini na baharini.