Rais Xi Jinping akutana na mawaziri wakuu wa Uholanzi na Sri Lanka
2024-03-28 08:24:45| CRI

Rais Xi Jinping wa China kwa nyakati tofauti amekutana na waziri mkuu wa Uholanzi Mark Rutte na waziri mkuu wa Sri Lanka Dinesh Gunawardena walioko ziarani mjini Beijing.

Kwenye mazungumzo na Bw. Rutte, Rais Xi amesema Uholanzi imekuwa lango halisi la ushirikiano kati ya China na Umoja wa Ulaya, na China iko tayari kudumisha mawasiliano na mazungumzo katika ngazi mbalimbali na Uholanzi, na kutafuta manufaa ya pamoja na matokeo ya kunufaishana.

Rais Xi amesema China inapenda kuongeza uagizaji wa bidhaa zenye ubora wa hali ya juu kutoka Uholanzi na kukaribisha kampuni za nchi hiyo kuwekeza nchini China, lakini pia ameeleza matumaini yake kuwa Uholanzi itatoa mazingira ya kibiashara yenye haki na uwazi kwa kampuni za China.

Alipokutana na waziri mkuu wa Sri Lanka Dinesh Gunawardena, Rais Xi amesema, kuimarisha na kukuza uhusiano kati ya China na Sri Lanka kunahudumia maslahi ya msingi na kuashiria matarajio ya pamoja ya watu wa nchi hizo mbili.

Rais Xi ameongeza kuwa China inapenda kushirikiana na upande wa Sri Lanka kuenzi moyo wa Mkataba wa Mpira kwa Mpunga, unaoashiria uhuru, umoja, kujitegemea na kuungana mkono, ili kuimarisha hali ya kuaminiana kisiasa, kuongeza mabadilishano ya uzoefu kwenye utawala wa nchi, kupanua ushirikiano wa kiutendaji na kuendeleza ushirikiano wa Ukanda Mmoja, Njia Moja.