Kenya yafikiria kupanua ufikiaji wa soko la mazao ya kilimo ili kuhimiza ukuaji wa uchumi
2024-03-28 08:34:05| CRI

Waziri Mkuu wa Kenya Bw. Musalia Mudavadi amesema Kenya imedhamiria kupanua ufikiaji wa soko la mazao yake ya kilimo, na kuongeza mapato ya fedha za kigeni na ukuaji wa uchumi.

Bw. Mudavadi ambaye pia ni waziri anayeshughulikia mambo ya kigeni na diaspora, amesema Kenya imeharakisha mabadiliko kutoka kilimo cha kujikimu kwenda cha kibiashara kama sehemu ya ajenda ya mabadiliko ya kiuchumi.

Akizungumza kwenye kongamano la siku mbili la ufadhili wa kilimo, Bw. Mudavadi pia amesema Kenya inafanya kazi na washirika wa kimataifa kupanua upatikanaji wa soko la bidhaa za kilimo za Kenya, na kuhimiza uwekezaji katika sekta hiyo.

Ametoa wito wa uwekezaji katika miundombinu, kama vile barabara za vijijini, hifadhi na mifumo ya umwagiliaji maji ili kupunguza upotevu wa mazao baada ya mavuno na kuboresha ufikiaji wa soko.