Serikali ya Kenya yasitisha mauzo ya mbolea aina ya NPK
2024-03-28 23:04:15| cri

Katibu wa Wizara ya Kilimo nchini Kenya, Dkt. Paul Rono, ameamuru kusitishwa kwa uuzaji wa mbolea aina ya NPK 10:26:10 inayotengenezwa na kampuni ya Ken Chemicals ya Thika.

Katika barua yake kwa Bodi ya Kitaifa ya Nafaka na Mazao (NCPB), Dkt Rono amesema uchunguzi uliofanywa na maafisa wa serikali katika mashamba umebaini kuwa mbolea hiyo haijatimiza viwango vinavyohitajika vya ubora. Ameitaka Bodi hiyo kufanya uchunguzi kubaini maelezo halisi kuhusu viungo na madini kwenye mbolea hiyo kabla ya kurejeshwa katika mpango wa serikali kwa utoaji mbolea kwa bei nafuu.

Dkt Rono alisema endapo itabainika kuwa mbolea hiyo haijatimiza matakwa na sifa zilizowekwa, kampuni iliyoitengeneza itaadhibiwa na kulazimishwa kugharimia hasara yote kwa serikali na wakulima.