Bodi kampuni tanzu ya TANESCO nchini Tanzania yavunjwa
2024-03-29 10:08:51| cri

Naibu Waziri Mkuu wa Tanzania na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko ameagiza kuvunjwa kwa bodi ya kampuni tanzu ya TANESCO ya Ujenzi na Ukarabati wa Miundombinu ya Usafirishaji na Usambazaji Umeme (ETDCO) kutokana na utendaji kazi mbovu, wizi fedha za umma ndani ya Shirika pamoja na wizi wa vifaa vya umeme uliokithiri, na kuagiza kuundwa upya kwa menejimenti ya kampuni hiyo.

Dk Biteko ametoa agizo hilo wakati wa kikao kazi kati yake na uongozi wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na kampuni zake tanzu, Wakurugenzi wa TANESCO wa Kanda na Mameneja wa Mikoa ambacho kilifanyika jana jijini Mwanza, kikiwa na lengo la kujadili utendaji kazi katika sekta ya umeme.

Hatua hii inakuja ikiwa ni siku moja baada ya Bodi ya TANESCO kuagizwa kumuondoa Meneja Mkuu wa ETDCO kutokana na utendaji mbovu wa kazi ndani ya taasisi na kusuasua kwa utekelezaji wa miradi ya umeme ukiwemo wa usafirishaji umeme kutoka Tabora hadi Urambo na Tabora hadi Mpanda.