Machi 30 kila mwaka ni Siku ya Madaktari, ambayo inatumika kukumbuka mchango wa Dokta Crawford Long, ambaye alifanikiwa kwa mara ya kwanza kufanya upasuaji kwa kutumia dawa ya usingizi, nah ii ilikuwa ni mwaka 1842. Madaktari kwa ujumla wamekuwa na kazi ngumu na nzito, na wamekuwa wakiitekeleza kwa moyo thabiti wa kujitolea, wakisaidia kutibu magonjwa aina mbalimbali, na hivyo kutoa mchango mkubwa katika ustawi wa jamii. Madaktari kotte duniani, ni jamii ya watu wanaoheshimika sana kutokana na kazi yao hii nzito wanayofanya, aidha wanapokuwa kwenye zamu katika vituo vya afya au hata wakiwa nje ya zamu. Udaktari ni fani ambayo mtu anakuwa kazini muda wote, bila kujali yuko hospitali, kwenye sherehe, ama sehemu yoyote ile.
Kwa upande wa madaktari wa kike, mara nyingi wamekuwa wakikabiliwa na changamoto mbalimbali katika utendaji wao wa kazi. Watu wengi wana Imani Zaidi na madaktari wa kiume kuliko wa kike, wakidhani kuwa, wanawake hawawezi kuwa na ujuzi sawa na madaktari wa kiume katika matibabu, jambo ambalo kimsingi tunaweza kusema kwamba, halina ukweli wowote. Tumewaona na kuwashuhudia madaktari wanawake wakifanya kazi sawa na hata kuwazidi wenzao wa kiume, hivyo mawazo kwamba madaktari wanawake ni dhaifu kuliko wenzao wa kiume hayana ukweli wowote. Katika kipindi cha Ukumbi wa Wanawake leo hii tutaangalia jinsi madaktari wa China wanavyofanya kazi katika nchi za Afrika na changamoto wanazokumbana nazo.