Balozi wa Iran nchini Syria aapa kulipiza kisasi kufuatia shambulio la Israel dhidi ya ofisi za ubalozi huo
2024-04-02 09:12:44| CRI

Balozi wa Iran nchini Syria Hossein Akbari ameapa kuwa Iran itatumia nguvu sawa kulipiza kisasi kufuatia shambulio la Israel dhidi ya ubalozi wa Iran ulioko mjini Damascus nchini Syria lililofanyika mapema jana.

Balozi Akbari amesema, wafanyakazi watano wa ubalozi wa Iran wameuawa kwenye shambulio hilo, na askari wawili wa ubalozi huo wamejeruhiwa. Amesema ni wazi kuwa Israel imekiuka sheria ya kimataifa, na kuonya kuwa Iran haitakaa kimya juu ya shambulio hilo na italijibu kwa nguvu sawa.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Syria Faisal Mekdad ameomboleza vifo vya watu hao, na kulaani mashambulizi hayo dhidi ya ofisi za kibalozi.