Njia ya reli ya kati ya Tanzania yapata ufadhili wa dola milioni 200 kutoka Benki ya Dunia
2024-04-02 10:12:44| cri

Sehemu ya reli ya kati ya Tanzania kutoka Dar es Salaam hadi Isaka nchini Tanzania iko tayari kufanyiwa maboresho makubwa kufuatia kuidhinishwa kwa ufadhili wa dola milioni 200 za kimarekani kutoka kwa Benki ya Dunia. Fedha hizo zimetengwa kwa ajili ya awamu ya pili ya Mradi wa Maendeleo ya Barabara na Reli Tanzania (TIRP-2), unaolenga kuimarisha usalama, kustahimili hali ya hewa, na ufanisi wa uendeshaji katika sehemu hiyo ya reli.

Vipengele muhimu vya mradi huo ni pamoja na kuimarisha miundombinu, ufanisi wa usafiri, kuimarisha ustahimilivu wa mabadiliko ya tabia nchi kwenye kipengele cha Kilosa-Gulwe-Igandu, usaidizi wa kiutendaji na kitaasisi, na uwezeshaji wa kukabiliana na dharura.

Takriban watu 900,000 wanatarajiwa kunufaika moja kwa moja na mradi huo, huku watu wengine milioni 3.5 wakinufaika kwa njia isiyo ya moja kwa moja, ambao ni takriban asilimia 5 ya watanzania wote.