Raia watatu wa kigeni wauawa katika mashambulio ya anga ya Israel katikati ya Ukanda wa Gaza
2024-04-02 09:10:47| CRI

Ofisi ya habari ya kundi la Hamas imesema, watu watano wameuawa katika shambulio la anga lililofanywa na jeshi la Israel katikati ya Ukanda wa Gaza, wakiwemo raia watatu wa kigeni.

Taarifa iliyotolewa na ofisi hiyo imesema, raia hao wa kigeni waliouawa walikuwa wafanyakazi wa shirika la kutoa misaada la "World Central Kitchen", na wanatokea Uingereza, Poland na Australia. Watu wengine wawili waliouawa katika shambulizi hilo la anga ni pamoja na raia mmoja wa Palestina na utambulisho wa mwengine bado haujathibitishwa. Hadi sasa Israel bado haijatoa tamko lolote kuhusu taarifa hiyo.

Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na idara ya afya ya Ukanda wa Gaza wa Palestina, operesheni za kijeshi za Israel katika eneo hilo katika saa 24 zilizopita zimesababisha vifo vya watu 63 na wengine 94 kujeruhiwa.