TRA yakusanya wastani wa Sh2.2 trilioni kwa mwezi
2024-04-03 10:53:57| cri

Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), imekusanya Shilingi trilioni 6.63 katika robo ya tatu ya mwaka wa fedha 2023/24, ikiwa ni ongezeko la asilimia 11.6 ya makusanyo ukilinganisha na kipindi kama hicho mwaka wa fedha uliopita. Katika mwaka wa fedha uliopita mamlaka hiyo ilikusanya shilingi trilioni 5.94.

Taarifa iliyotolewa na TRA na kusainiwa na Kamishna wa mamlaka hiyo Bw. Alphayo Kidata inaeleza kiasi hicho kilichokusanywa ni ufanisi wa asilimia 95.17. Mchanganuo wa makusanyo hayo kwa kila mwezi unaonyesha Machi, mwaka huu mamlaka hiyo imekusanya shilingi trilioni 2.49 chini ya lengo la kukusanya shilingi trilioni 2.56.

Mwezi Februari TRA ilikusanya shilingi trilioni 2.02 chini ya lengo la kukusanya Shilingi trilioni 2.1 sawa na ufanisi wa asilimia 93, huku Januari ikikusanya Shilingi trilioni 2.12, sawa na ufanisi wa asilimia 94.4. Kwa mujibu wa TRA, kilichohimiza makusanyo hayo ni kuongezeka kwa uhiari wa ulipaji kodi, mwitikio mzuri wa walipa kodi na kuongezeka kwa ufanisi katika huduma za forodha.