UM walaani shambulio dhidi ya Ubalozi wa Iran nchini Syria
2024-04-03 09:24:58| CRI

Umoja wa Mataifa umelaani vikali tuhuma zilizotolewa na Iran kwamba Israel imeshambulia eneo la ubalozi wake nchini Syria kwa makombora na kusababisha vifo na majeruhi ya watu.

Msaidizi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Khaled Khiari amesema kwenye mkutano wa dharura wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu shambulio la Israel katika ubalozi wa Iran nchini Syria, kuwa limesababisha vifo vya wafanyakazi watano raia wa Iran, wakiwemo washauri waandamizi wa kijeshi.

Ametoa wito wa kujizuia na kudumisha sheria ya kimataifa, ikiwemo ulinzi wa raia na miundombinu, na kujaribu kukwepa mgogoro huo kuenea zaidi ukiwa na athari kubwa kwa watu ambao tayari wanakabiliwa na hali ngumu katika kanda ya Mashariki ya Kati.

Wakati huohuo, rais Bashar al-Assad wa Syria ametoa salamu za rambirambi kwa mwenzake wa Iran Ebrahim Raisi kufuatia vifo vya washauri waandamizi wa kijeshi wa Iran katika shambulio la Israel dhidi ya Ubalozi wa Iran nchini Syria.

Katika mzungumzo yao kwa njia ya simu, rais Assad ameilaumu Israel kwa kuendeleza vurugu katika kanda hiyo, na kuchukulia mapigano yanayoendelea Gaza kama ushahidi wa nia ovu ya Israel.