China na Tanzania zawakumbuka wataalamu wa China waliofariki wakati wa ujenzi wa reli ya TAZARA
2024-04-03 09:30:42| CRI

Wafanyakazi wa ubalozi wa China nchini Tanzania, wajumbe wa makampuni na jamii ya China pamoja na maofisa wa serikali ya Tanzania Jumanne walifanya ibada ya kuwakumbuka raia wa China waliofariki wakati wa ujenzi wa reli ya TAZARA katika miaka ya 70 ya karne iliyopita.

Balozi wa China nchini Tanzania Chen Mingjian na Waziri wa Uchukuzi wa Tanzania Makame Mbarawa walishiriki kwenye shughuli hiyo, wakiweka shada la maua kwenye makaburi yaliyoko Gongo la Mboto pembezoni mwa jiji la Dar es Salaam.

Balozi Chen amesema marehemu hao ni mashujaa waliojenga mnara wa urafiki kati ya China na Tanzania na kati ya China na Afrika, na kwamba reli ya TAZARA inaonyesha kuheshimiana, kutendeana kwa usawa, uvumilivu na moyo wa kimataifa.

Kwa upande wa Tanzania, Waziri Mbarawa amesema Watanzania hawatasahau kamwe wataalamu hao wa China na mchango uliotolewa nao kwenye sekta ya maendeleo ya kiuchumi.