Rais Xi Jinping atoa heshima kwa mashujaa na mashahidi
2024-04-03 10:09:40| cri

Methali ya Kiswahili inasema “Mwili hupotea, lakini roho hubaki.” Aprili 4 ni Siku ya kuwakumbuka marehemu ya China, ambayo ni siku ya jadi ya Wachina kuwakumbuka ndugu walioaga dunia. Akiwa Rais wa China na Katibu Mkuu wa Kamati Kuu ya Chama cha Kikomunisti cha China (CPC), Bw. Xi Jinping kwa nyakati tofauti ameonesha heshima mara nyingi kwa watangulizi wa mapinduzi na mashahidi waliotoa mchango mkubwa katika kupigania uhuru wa taifa, ukombozi wa watu, ustawi wa nchi na maisha bora ya wananchi.

Akiwakumbuka watangulizi wa mapinduzi, Rais Xi amesema, tangu CPC kilipoasisiwa hadi Jamhuri ya Watu wa China ilipoanzishwa, idadi ya mashahidi waliorekodiwa majina yao imezidi milioni 3.7, huku idadi ya wale ambao majina yao hayakurekodiwa ikiwa haihesabiki, mashujaa hawa walijitoa muhanga ili kutekeleza majukumu kwa taifa na wananchi.
Kwa maofisa na askari wa Jeshi Jekundu, Rais Xi amesema, wanajeshi hao hawakuogopa vifo wakiwa na ushupavu na ujasiri wa kusonga mbele na kushinda taabu na changamoto yoyote iliyowakabili, wanastahili kukumbukwa na kuenziwa daima.

Akiwataja wanajeshi waliojitolea kuisaidia Korea Kaskazini kupambana na uvamizi wa Marekani, Rais Xi amesema, siku zote hatuwezi kuwasahau mashahidi waliopoteza maisha katika vita ya Korea Kaskazini dhidi ya uvamizi wa Marekani, watu mashujaa zaidi ya 197,000 walijitoa muhanga kwa ajili ya taifa, kwa ajili ya wananchi na kwa ajili ya amani.