Wataalamu wakutana nchini Kenya kujadiliana njia za kuimarisha ushirikiano katika usimamizi wa mipaka barani Afrika
2024-04-03 09:21:57| CRI

Wataalamu wa uhamiaji wameanza mkutano wa siku tatu mjini Nairobi, Kenya, kujadili njia za kuimarisha ushirikiano katika usimamizi wa mipaka barani Afrika.

Mkutano huo unaofanyika chini ya kaulimbiu “Kujenga uratibu kuelekea maingiliano,” umewakutanisha zaidi ya washiriki 300 kutoka Umoja wa Mataifa na maofisa waandamizi wa usimamizi wa mipaka barani Afrika, na unatumika kama jukwaa la majadiliano, ushirikiano na uvumbuzi katika usimamizi wa mipaka barani humo.

Mkuu wa Tume ya Shirika la Kimataifa la Uhamiaji nchini Kenya, Dimanche Sharon amesema, bara la Afrika limejizatiti katika kuboresha uratibu bora wa mifumo ya usimamizi wa mipaka katika maeneo yote ya kuingia na kutoka katika nchi za bara hilo.

Waziri wa Mambo ya Ndani wa Kenya, Kithure Kindiki amesema, ushirikiano kati ya nchi za Afrika kupitia mabadilishano ya taarifa unatarajiwa kumaliza biashara ya bidhaa haramu katika mipaka ya nchi hizo.