Bandari ya kwanza ya uvuvi nchini Tanzania kukamilika mwaka 2025
2024-04-04 08:56:46| CRI

Waziri Mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa amesema, ujenzi wa bandari ya kwanza ya uvuvi nchini humo utakamilika mwaka 2025 na hivyo kuboresha uvuvi wa bahari ya kina kirefu nchini humo.

Akizungumza katika mkutano wa Bunge la Tanzania mjini Dodoma, Waziri Mkuu Majaliwa amesema ujenzi wa bandari hiyo unaofanyika Kilwa Masoko katika ufukwe wa Bahari ya Hindi umefikia asilimia 42.

Kwa mujibu wa Mamlaka ya Bandari nchini Tanzania, mradi huo unatekelezwa na kampuni ya Uhandisi wa Bandari ya China (CHEC), na umesaidia zaidi ya watu 400 wa huko kupata ajira.

Makamu mkuu wa kampuni hiyo tawi la Afrika Mashariki Tang Zhen amesema, kampuni hiyo itafanya kila linalowezekana kuisaidia Tanzania kujenga bandari ya kwanza ya uvuvi, hivyo kuimarisha zaidi urafiki na ushirikiano kati ya China na Tanzania.