Mshauri wa masuala ya nishati endelevu katika Shirika la Afya Duniani (WHO) Salvatore Vinci amesema, upatikanaji wa umeme katika vituo vya afya kwenye maeneo ya vijijini katika nchi za Afrika kusini mwa Sahara ni ufunguo wa uwezo wa bara hilo kukabiliana na milipuko ya magonjwa.
Amesema kutimiza afya kwa wote barani Afrika na eneo kubwa la nchi za Kusini kutategemea katika upatikanaji wa umeme katika vituo vya afya ili kusaidia uhifadhi wa chanjo na matumizi ya mashine za kugundua magonjwa. Amezitaka serikali, wawekezaji na wafadhili kupunguza pengo la upatikanaji wa umeme kupitia uvumbuzi wa ufadhili, sera na mageuzi ya kanuni ili kuwezesha Afrika kupata huduma bora za afya.
Amesema katika eneo la Afrika kusini mwa Sahara, asilimia 15 ya vituo vya afya havina umeme, na hivyo kuathiri juhudi za kupunguza mzigo wa magonjwa unaotokana na umasikini na mabadiliko ya tabianchi.