Mafunzo ya usalama wa kidijitali ya TikTok yawawezesha wakenya 116,000
2024-04-05 09:51:21| CRI

Jukwaa la video fupi la TikTok limesema, mafunzo ya usalama wa kidijitali yaliyofanywa pamoja na kampuni ya utatuzi wa mawasiliano ya Eveminet yenye makao makuu huko Nairobi, Kenya, yamewawezesha wakenya 116,000 tangu mwezi wa Oktoba mwaka 2023.

Mkurugenzi wa sera za serikali na umma wa TikTok kanda ya Afrika kusini mwa Jangwa la Sahara, Bw. Fortune Mgwili-Sibanda amesema, mafunzo hayo yameshirikisha washiriki wengi wakiwemo wanafunzi, wazazi na walimu kutoka kaunti 21 kati ya kaunti 47 za Kenya, ambao wamenufaika na masomo yanayowawezesha kuwa ujuzi wa usalama wa kidijitali ndani ya kaunti zao.

Mgwili-Sibanda amesema, tangu mwezi Aprili hadi Septemba mwaka 2024, wanalenga kutoa mafunzo hayo kwenye kaunti nyingine 26, ili kuwezesha nchi nzima kupata elimu ya lazima ya usalama wa kidijitali.