Ethiopia na nchi nyingine za Afrika zimetakiwa kujifunza uzoefu wa China kutokana na mafanikio ya nchi hiyo katika kupunguza umasikini, ikiwa ni sehemu ya juhudi zao za kuhimiza maendeleo ya uchumi na kuwaondoa mamilioni ya watu katika umasikini.
Taarifa iliyotolewa hivi karibuni na kumnukuu mkuu wa idara ya uhusiano wa umma na kimataifa wa chama tawala cha Ustawi nchini Ethiopia, Addisu Arega, imesema ujumbe wa ngazi ya juu wa wanachama wa Chama hicho uko nchini China kujifunza kivitendo, ambapo wamekagua juhudi za China za kuondokana na umasikini na uzoefu wa jumla wa nchi hiyo.
Ujumbe huo umesisitiza kwamba mafanikio makubwa ya China katika kuondokana na umasikini, maendeleo ya mazingira katika kubadili maeneo ya jangwa kwa kufanya uratibu na watu, pamoja na mafanikio yaliyopatikana katika kujenga umoja wa kitaifa ili kuongeza kasi ya maendeleo, ni baadhi ya maeneo ambayo Ethiopia inaweza kujifunza.