Serikali ya Tanzania kuongeza vituo vinavyotoa mionzi kwa wagonjwa wa saratani
2024-04-08 13:52:53| cri

Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Afya inaendelea na taratibu za uwekezaji kwa kuongeza vituo vingine vinne kwa kujenga majengo na kuviwezesha vifaa vitakavyotumika kutibu wagonjwa wa Saratani kwa njia ya mionzi.

Hayo yamesemwa hivi karibuni na Waziri wa Afya wa nchi hiyo, Ummy Mwalimu katika mkutano wa Bunge la nchi hiyo unaoendelea mjini Dodoma. Waziri Ummy amesema, kwa sasa serikali ina jumla ya vituo vinne ambavyo vinatoa huduma ya matibabu ya Saratani nchinihumo  kwa njia ya Mionzi, ambavyo ni Taasisi ya Saratani Ocean Road, Hospitali ya Kanda Bugando, Hospitali ya binafsi Besta na Hospitali ya Good Sammaritan ya Ifakara.

Amesema serikali inaendelea na taratibu za uwekezaji kwa kuongeza vituo vingine vinne vya kutoa tiba hiyo katika Hospitali ya Benjamin Mkapa, KCMC, Hospitali ya Rufaa ya Kanda Mbeya na Hospitali binafsi ya Agakhan kwa Tanzania bara, na Hospitali ya Binguni Visiwani Zanzibar.