Rwanda yaeleza wasiwasi wake kufuatia Marekani kuwa na utata kuhusu watu waliouawa katika mauaji ya kimbari ya mwaka 1994
2024-04-09 08:44:52| CRI

Rais wa Rwanda Paul Kagame ameeleza wasiwasi wake kutokana na Marekani kuwa na utata kuhusu watu waliouawa katika mauaji ya kimbari ya mwaka 1994 nchini Rwanda.

Kauli hiyo ya rais Kagame imekuja baada ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Anthony Blinken kutuma ujumbe katika maadhimisho ya kumbukumbu ya miaka 30 ya mauaji ya kimbari ya Rwanda kupitia mtandao wa kijamii wa X, akisema “wanasikitishwa na vifo vya Watutsi, Wahutu, Watwaa na wengine waliopoteza maisha katika siku 100 za vurugu kubwa”.

Akizungumza katika mkutano na wanahabari jijini Kigali hapo jana, rais Kagame amesisitiza kuwa, suala hilo lilijadiliwa na rais wa zamani wa Marekani Bill Clinton, ambaye aliongoza ujumbe wa Marekani katika kumbukumbu ya miaka 30 ya mauaji ya kimbari ya Rwanda iliyofanyika jumapili iliyopita mjini Kigali.

Akizungumza wakati wa maadhimisho ya kumbukumbu hiyo, Rais Kagame amesema Wanyarwanda hawataelewa ni kwa nini baadhi ya nchi zinaendelea kuwa na utata kuhusu nani alilengwa katika mauaji hayo ya kimbari, na kusema kufanya hivyo ni aina ya kukataa kile kilichotokea, na huo pia ni uhalifu.