Umoja wa Afrika watafuta fedha kuunga mkono jukumu la ufuatiliaji nchini Somalia kwa mwaka 2025
2024-04-09 08:52:46| CRI

Tume ya Amani na Usalama ya Umoja wa Afrika (AUPSC) imetoa wito wa ufadhili kamili, endelevu na wa wakati kwa ajili ya tume itakayoanzishwa hivi karibuni ya ufuatiliaji baada ya Tume ya Mpito ya Umoja huo nchini Somalia (ATMIS) kuondoka nchini humo mwezi Desemba mwaka huu.

Taarifa iliyotolewa na Tume hiyo jana imesema, inakaribisha pendekezo lililotolewa na serikali ya Somalia la kuomba mpangilio wa usalama baada ya ATMIS kuondoka nchini humo, na ombi la Somalia la kuanzisha kikosi cha kulinda amani kinachoongozwa na Umoja wa Afrika na kuungwa mkono na Umoja wa Mataifa kitakachochukua nafasi ya ATMIS kuanzia Januari Mosi, 2025.

ATMIS inatarajiwa kuondoka nchini Somalia mwezi Desemba mwaka huu, lakini hata hivyo, maandalizi yanaendelea kupeleka kikosi kingine kinacholenga kudumisha maendeleo yaliyopatikana hadi sasa na kasi inayoendelea katika kupambana na kundi la al-Shabaab linalotaka kuipindua serikali ya Somalia.