Jeshi la Polisi nchini Tanzania limethibitisha kutokea kwa vifo vya watu 15 ambao wamesombwa na maji kufuatia mvua znazoendelea kunyesha katika maeneo mbalimbali nchini humo, ambapo kati ya watu hao, 12 ni watoto na watatu ni watu wazima.
Taarifa iliyotolewa na Jeshi hilo imesema, watu hao wengine walifariki wakiwa wanaogelea, wengine wakiwa wanavuka maeneo ambayo maji yanatiririka kwa kasi na wengine kutokana na kutumbukia kwenye mashimo ama madimbwi yaliyojaa maji.
Jeshi hilo limesema, matukio hayo yametokea katika wilaya mbalimbali nchini humo, ambapo katika wilaya ya Kalambo Mkoa wa Rukwa, mtu mmoja mwanaume wa miaka 18, alisombwa na maji ya mvua yaliyokuwa yakitokea milimani wakati akijaribu kuvuka daraja Aprili 1, 2024.