Kenya iko hali ya tahadhari kukabiliana na matishio ya kigaidi
2024-04-09 08:45:34| cri



Serikali ya Kenya jana imesema kuwa vyombo vyake vya usalama viko katika hali ya tahadhari kukabiliana na matishio ya kigaidi kote nchini. 

Katibu mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani na Utawala wa Kitaifa Raymond Omollo, amesema licha ya matukio machache yaliyoripotiwa katika mpaka wa Kenya na Somalia, nchi hiyo kwa ujumla iko salama. 

Kauli yake hiyo imefuatia ushauri wa tahadhari ya usafiri uliotolewa na Uingereza na Australia wikiendi iliyopita, ambazo zilionya kuongezeka kwa mashambulio ya ugaidi yanayolenga raia wa kigeni nchini Kenya. Katika kujibu onyo hilo, polisi wa Kenya waliwahakikishia Wakenya na raia wa kigeni kuwa hakuna haja ya hofu, kwani wamechukua hatua za kukabiliana na matishio hayo.