Chuo Kikuu cha Kilimo cha China chaandaa mdahalo wa masuala ya kilimo na wataalamu kutoka Tanzania
2024-04-10 14:36:20| Cri

Chuo Kikuu cha Kilimo cha China mjini Beijing, kimeandaa mdahalo maalum wa China na Tanzania kwa lengo la kubadilishana uzoefu na kutafuta njia za maendeleo zaidi katika sekta ya kilimo kati ya nchi hizo.

Mkuu wa Mkoa wa Morogoro nchini Tanzania, ambaye ameongoza ujumbe wa Tanzania katika mdahalo huo, Adam Kigoma Malima, amesema, kupitia ushirikiano na China, anatumai kuwa Tanzania itaweza kufikia mafanikio makubwa ya kilimo kutokana na utayari wa China wa kupeleka wataalamu wa kilimo na teknolojia mpya za kisasa, ambazo ni nyenzo muhimu katika mageuzi ya kilimo.

Pia Bw. Malima amesema, hatua ya China kuhamisha teknolojia zake za kilimo kwa nchi nyingine zinazoendelea ikiwemo Tanzania, imesaidia wakulima kuongeza mavuno ya mazao yao na kujiongezea kipato.

Akiuzungumzia miaka 60 ya uhusiano wa kidiplomasia kati ya Tanzania na China, Bw. Malima amesema Tanzania imenufaika sana na uhusiano huo, hususan katika sekta za afya, miundombinu, elimu, biashara na uchumi.