Sudan Kusini imetangaza kuwa itaanza maandalizi ya uchaguzi wa wabunge uliopangwa kufanyika mwezi Desemba mwaka huu, ukiwa ni wa kwanza tangu nchi hiyo ipate uhuru wake.
Kufuatia kumalizika kwa vita ya wenyewe kwa wenyewe mwaka 2018 na kupata uhuru wake mwaka 2011, Sudan Kusini awali ilipanga kufanya uchaguzi kabla ya mwezi Februari mwaka jana, lakini serikali ya mpito ya nchi hiyo na upande wa upinzani walikubaliana kuahirisha hadi mwishoni mwa mwaka 2024.
Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi ya Sudan Kusini Abednego Akok Kacuol amewaambia wanahabari jijini Juba kuwa, serikali imetoa fedha kwa Tume hiyo kuanza mchakato wa uchaguzi, na kwamba wameandaa mpango ambao kama utaridhiwa na wadau, uandikishaji wapiga kura utaanza mwezi Juni.