Marekani yatakiwa kuwajibika kihalisi baada ya ziara ya Bi. Yellen nchini China
2024-04-10 11:10:24| cri

Waziri wa Fedha wa Marekani Bi. Janet Yellen jana amemaliza ziara yake nchini China, akiwa ni mjumbe wa kwanza wa baraza la mawaziri la Marekani kufanya ziara nchini China mwaka huu, pia ikiwa ni ziara ya pili nchini China baada ya miezi tisa.

Wakati wa ziara yake, pande mbili zimefanya mawasiliano ya ngazi na sekta mbalimbali, huku zikikubaliana kutekeleza kwa pamoja makubaliano muhimu yaliyofikiwa na marais wa nchi mbili na kufikia makubaliano mapya katika upande wa kuhimiza ukuaji wa uchumi na ushirikiano wa kifedha. Bi. Yellen amesema, China na Marekani zinatakiwa kuwajibika kwa pamoja kwenye uhusiano wa kiuchumi wa pande mbili, huku akisisitiza tena kutotafuta kutengana na China kiuchumi.

Hoja ya Yellen ya kusisitiza uwajibikaji inasikika kuwa nzuri, lakini hakuna mtu anayejua jinsi Marekani itakavyowajibika kivitendo. Kwa sababu ukweli ni kwamba, vikwazo vya Marekani vinavyolenga uchumi, biashara, sayansi na teknolojia za China, na orodha ya kuweka vizuizi dhidi ya makampuni ya China inazidi kuwa ndefu. China na Marekani ni nchi kubwa zaidi kiuchumi duniani, na China siku zote inaona kuwa msingi wa ushirikiano wa kiuchumi na kibiashara kati yake na Marekani ni wa kunufaishana, huku ikifanya juhudi kuelekea mwelekeo huo.

Bi. Yellen ametaja uwajibikaji, hivyo kuna haja ya kueleza bayana maana halisi ya kuwajibika. Kwanza, Marekani haiwezi kuyafanya mambo ya kiuchumi na kibiashara kuwa suala la kisiasa. Juu ya msingi huu, ushirikiano wa kiuchumi na kibiashara kati ya China na Marekani unatakiwa kufanyika kwa kufuata kanuni za uchumi na soko.

Mwaka huu ni maadhimisho ya miaka 45 tangu China na Marekani zianzishe uhusiano wa kibalozi. Historia imethibitisha kuwa, maslahi ya kiuchumi kati ya China na Marekani yameungana kwa kina, kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi na kibiashara kunanufaisha pande mbili, pia kunanufaisha ukuaji wa uchumi wa dunia nzima.