China na Russia zafungua njia mpya ya nchi kubwa na jirani kuishi pamoja kwa amani na kunufaishana
2024-04-10 11:07:12| cri

Rais wa China Xi Jinping jana hapa Beijing alikutana na Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia Sergey Lavrov.

Katika mazungumzo yao, Rais Xi amesema huu ni mwaka wa 75 tangu kuanzishwa kwa uhusiano wa kibalozi kati ya China na Russia, na kwamba hizo mbili zimefungua njia mpya ya nchi kubwa na jirani kuishi pamoja kwa amani na kunufaishana. Rais Xi amesema mwezi Februari mwaka huu, aliongea kwa njia ya simu na rais Vladmir Putin wa Russia, na kuweka mipango mipya juu ya maendeleo ya uhusiano kati ya nchi mbili. Viongozi hao walikubaliana kufanya mazungumzo na uratibu kwa wakati juu ya masuala ya kimkakati, kutoa kipaumbele kwa masuala yanayohusu uhusiano kati ya pande mbili na mambo ya kikanda na kimataifa, na kuhakikisha uhusiano kati ya China na Russia unaendelea vizuri kwa utulivu siku zote.

Kwa upande wake, Bw. Lavrov amefikisha salamu za rais Putin kwa rais Xi, na kusema Russia inapenda kushirikiana na China katika kutekeleza vizuri kazi mpya za kimkakati zilizotolewa na wakuu wa nchi mbili.