Uharamia waendelea kuwa tishio katika bahari ya Somalia
2024-04-11 08:37:19| CRI

Mashambulio yanayofanywa na maharamia katika bahari karibu na Somalia yameendelea kuwa tishio, wakati matukio mawili ya utekaji wa meli yakiripotiwa katika robo ya kwanza ya mwaka huu.

Ripoti iliyotolewa na Shirika la Kimataifa la Mambo ya Baharini (IBM) lililo chini ya Shirikisho la Kimataifa la Biashara (ICC) imetoa wito kwa meli zinazopita katika pwani ya Somalia na Ghuba ya Aden kuwa waangalifu kwa kuwa uharamia bado ni tishio licha ya kupungua kwa mashambulio tangu mwaka 2017.

Katibu Mkuu wa ICC John Denton amesema, kuibuka tena kwa shughuli za uharamia unaofanywa na Wasomali kunaleta wasiwasi, na ni muhimu sana kwa sasa kulinda biashara, kulinda njia za meli na kuhakikisha usalama wa wasafiri wa baharini wanaoendeleza biashara.