Umoja wa Mataifa watoa wito wa kuongezwa kwa uwekezaji wa kifedha ili kufikia Malengo ya Maendeleo Endelevu
2024-04-11 08:34:28| cri

Ripoti iliyotolewa jumanne wiki hii na Umoja wa Mataifa imesema, uhamasishaji mkubwa wa kifedha unahitajika haraka ili "kuokoa" Malengo ya Maendeleo Endelevu ya Umoja wa Mataifa ambayo kwa sasa yanakabiliwa na changamoto, na kujaza pengo la sasa la ufadhili wa maendeleo la dola za kimarekani trilioni 4.2 kwa mwaka.

Ripoti hiyo inayoitwa "Ripoti ya Ufadhili wa Maendeleo Endelevu ya mwaka 2024: Ufadhili wa Maendeleo katika Njia Mpanda," inaeleza kuwa kwa upande mmoja, kufikia Malengo ya Maendeleo Endelevu ya Umoja wa Mataifa kunakabiliwa na pengo la ufadhili wa maendeleo. Kwa upande mwingine, kuongezeka kwa mivutano ya siasa za kijiografia, mabadiliko ya tabianchi yanayosababisha maafa ya mara kwa mara, na kupanda kwa gharama ya maisha vimeathiri mabilioni ya watu duniani kote, na kukwamisha maendeleo katika huduma za afya, elimu na malengo mengine ya maendeleo ya Umoja wa Mataifa.