Maonyesho ya Soko la Utalii la Dunia la Afrika mwaka 2024 lafunguliwa Afrika Kusini
2024-04-11 08:36:46| CRI

Toleo la 10 la Maonyesho ya Soko la Utalii la Dunia mwaka 2024 limeanza jana jumatano mjini Cape Town, Afrika Kusini, na kuwakutanisha watu maarufu katika sekta ya usafiri na utalii kwa lengo la kujadili fursa za biashara katika sekta ya utalii.

Maonyesho hayo yanayofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Cape Town, yanaonyesha umuhimu wa fursa za utalii katika kanda hiyo kupitia mfululizo wa burudani, mikutano, na hafla za utoaji wa tuzo.

Waandaaji wa maonyesho hayo wamesema, ikiwa sehemu ya Wiki ya Usafiri ya Afrika 2024 iliyoanza tarehe 7 hadi 12 mwezi huu mjini Cape Town, shughuli hiyo imeandaliwa ili kuboresha ufahamu wa sekta ya utalii, kuongeza mawasiliano, na kuboresha ukuaji wa biashara. Pia shughuli hiyo inatoa fursa kwa mashirika ya ndege, kampuni za meli za utalii, mahoteli na wakala wa usafiri kuonyesha huduma zao bora kwa jamii ya kimataifa.