Umoja wa Mataifa wasema mgogoro nchini Sudan umesababisha vifo vya maelfu ya watu
2024-04-12 09:31:05| cri



Msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Bw. Stephane Dujarric, jana amesema, ripoti iliyotolewa na ujumbe wa Umoja huo nchini Sudan imeonesha kuwa, mgogoro ulioanza Aprili 15 mwaka jana kati ya jeshi la Sudan na kikosi cha RSF umesababisha vifo vya maelfu ya watu huku mamilioni wengine wakikimbia makazi yao.

Amesema watu zaidi ya milioni 6 nchini Sudan wamekimbia makazi yao, huku karibu wakimbizi milioni 2 wakikimbilia katika nchi jirani, na watu milioni 24 wanahitaji msaada.

Bw. Dujarric pia amesema, Ufaransa, Ujerumani na Umoja wa Ulaya zitaitisha mkutano wa msaada wa kibinadamu kwa Sudan na nchi jirani zake Jumatatu ijayo huko Paris, ambapo watazungumzia kuongeza rasilimali ili kupanua operesheni za misaada nchini Sudan na nchi nyingine za kanda hiyo.